Karibu kwenye ulimwengu wa elimu ya juu! Chuo kikuu ni mahali ambapo "kusoma kwa bidii" (hard work) pekee hakutoshi; unahitaji kusoma kwa akili (smart work). Tofauti na sekondari, huku mwalimu hakuandikii notisi ubaoni. Wewe ndiye dereva wa masomo yako. Hebu kwa nza tuangalie nini maana ya usomaji, hasa usomaji wenye tija katika elimu ya juu.
Neno "Usomaji" linatokana na neno soma ambalo maana yake ni fahamu yaliyoandikwa kwa kutamka, kupitisha macho au kugusa kama vile maandishi ya walemavu wa macho. Lakini maana ya pili ya neno soma ni pata elimu, elimu hii unaweza kuipata shuleni, chuoni au mahali pengine kwa namna tofauti tofauti.
Usomaji ni hali ya kusoma maandishi, hasa ya vitabu vilivyoandikwa na wanadamu wengine. Maarifa hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kupelekea mwanadamu kutafuta maarifa naye mwenyewe kuandika vitabu mbalimbali. Hivyo Usomaji wenye tija ni hali au kitendo cha kusoma kitabu, makala au maandiko mbalimbali nakupata matokeo mazuri na yenye faida.
Kufaulu katika elimu ya juu si jambo la kubahatisha; ni matokeo ya hali fulani ya kisaikolojia, kimazingira na kimbinu ambayo mwanafunzi anapaswa kujiwekea. Chuo kikuu kinahitaji mabadiliko makubwa ya mfumo wa maisha kuliko ilivyokuwa sekondari
Hali ya Kisaikolojia (Mindset)
Ufaulu unaanzia kichwani. Mwanafunzi anayefaulu anapaswa kuwa na:
Nidhamu Binafsi (Self-Discipline): Chuo kuna uhuru mwingi. Hali ya usomaji inayofaa ni ile ambapo unajua wakati wa kuburudika na wakati wa kukaa maktaba bila kusukumwa na mwalimu au mzazi.
Udadisi wa Kitaaluma: Usisome ili upate "Pass". Soma ili uelewe fani yako. Hii inapunguza shinikizo la mitihani na kuifanya elimu kuwa sehemu ya maisha yako.
Kujiamini: Kuamini kuwa unaweza kuelewa mada ngumu (kama vile Calculus au Sheria za Mikataba) ni hatua ya kwanza ya kufungua uwezo wa ubongo wako.
Hali ya Mazingira (Environment)
Mazingira unayosomea yanaathiri asilimia kubwa ya kile unachohifadhi:
Utulivu wa Macho na Masikio: Tafuta mahali pasipo na kelele na pasipo na mivuto ya upotezaji muda (distractions) kama TV au watu wanaopiga soga.
Mpangilio wa Vifaa: Dawati lililojaa takataka huchosha akili haraka. Hakikisha sehemu yako ya kazi ni safi na ina vifaa vyote (kalamu, karatasi, laptop) ili usikatize usomaji wako kufuata kitu.
Nuru na Hewa: Usisome kwenye giza au chumba chenye joto kali. Hali hizi huleta uchovu na usingizi mapema.
Hali ya Mbinu (Study Strategy)
Kufaulu chuo kunategemea jinsi unavyocheza na "Data" unazopewa:
Kuhudhuria Mihadhara (Lectures): Hali bora ya usomaji huanza darasani. Profesa anapofundisha, anatoa "clues" za nini ni muhimu. Kukosa vipindi ni kujitengenezea mzigo mkubwa wa kusoma peke yako baadaye.
Majadiliano ya Vikundi (Group Discussions): Elimu ya juu inahitaji kubadilishana mawazo. Kusoma na wenzako kunakusaidia kuona mapungufu yako na kuelewa mada kwa mitazamo tofauti.
Kufanya Tafiti za Ziada: Usitegemee "Handouts" pekee. Tumia vyanzo kama Google Scholar, majarida ya kisayansi, na maktaba ya mtandao ili kuwa na hoja mbalimbali kwenye majibu yako ya mtihani.
Hali ya Afya na Ustawi (Well-being)
Huwezi kufaulu ikiwa mwili wako umechoka:
Usingizi wa Kutosha: Ubongo unahitaji muda wa kupanga taarifa ulizosoma (Memory Consolidation). Kukesha (kufanya "Tigo") mara nyingi hupunguza uwezo wa kufikiri sawasawa wakati wa mtihani.
Lishe na Maji: Kunywa maji mengi husaidia ubongo kufanya kazi kwa haraka. Epuka kusoma ukiwa na njaa kali au ukiwa umekula kupita kiasi (chakula kizito huleta uvivu).
Je, unahisi kulemewa na mada nyingi? Je, mtihani ukikaribia unapaniki? Usijali. Hapa kuna mbinu zitakazokusaidia siyo tu kufaulu, bali kuelewa kile unachokisoma.
Mbinu ya Pomodoro (Udhibiti wa Muda)
Wanafunzi wengi hujaribu kusoma kwa saa tano mfululizo, jambo ambalo huchosha ubongo. Mbinu ya Pomodoro inakushauri: usome kwa dakika 25.Pumzika kwa dakika 5 (nyoosha viungo, kunywa maji). Rudia mzunguko huo mara nne, kisha chukua mapumziko marefu ya dakika 15-30.
Faida: Hii inasaidia ubongo wako kubaki na umakini (focus) wa hali ya juu bila kuchoka haraka.
Mbinu ya Feynman (Fundisha ili Uelewe)
Mwanafizikia Richard Feynman aliamini kuwa kama huwezi kuelezea kitu kwa lugha rahisi, basi hukielewi vizuri. Chukua mada uliyoisoma, kisha jaribu kumuelezea rafiki yako (au hata ukuta!) kana kwamba ni mtoto wa miaka 10. Sehemu utakayokwama ndiyo sehemu ambayo bado hujaielewa vizuri. Rudi kwenye vitabu na uisome tena.
Active Recall na Spaced Repetition
Badala ya kusoma notisi zako mara kwa mara (Passive Reading), jaribu kujipa maswali.
Active Recall: Baada ya kusoma ukurasa mmoja, funga kitabu na ujiulize: "Nimejifunza nini hapa?"
Spaced Repetition: Usisome mada moja leo na kuiacha mpaka mwezi ujao. Isome leo, baada ya siku mbili, baada ya wiki moja, na baada ya mwezi mmoja. Hii inahamisha taarifa kutoka kwenye kumbukumbu ya muda mfupi kwenda kwenye kumbukumbu ya muda mrefu.
Boresha Mazingira Yako ya Usomaji
Simu yako ndiyo adui mkubwa wa "GPA" yako. Weka simu mbali au tumia "Focus Mode". Tafuta sehemu yenye mwanga wa kutosha na hewa safi (Library au sehemu tulivu). Hakikisha una vifaa vyote unavyohitaji (kalamu, maji, vitabu) kabla ya kuanza ili usipoteze muda kunyanyuka mara kwa mara.
Tumia Michoro na "Mind Maps"
Ubongo wa binadamu unakumbuka picha haraka kuliko maandishi matupu. Unaposoma mada pana, itengenezee mchoro (diagram) unaoonyesha jinsi mawazo yanavyoungana. Hii inasaidia kuona picha kubwa ya somo husika.
Hitimisho
Kufaulu chuo kikuu siyo uchawi; ni nidhamu na matumizi ya mbinu sahihi. Kumbuka, afya yako ni muhimu pia. Lala masaa 7-8, kula mlo kamili, na usisahau kufanya mazoezi kidogo.
Je, wewe unatumia mbinu gani unaposoma? Tuambie kwenye maoni hapo chini!


0 Comments